A person who knows and is aware that he knows, is wise, follow him; A person who knows but is not aware that he knows, remind him; A person who doesn't know and is aware that he doesn't know, teach him; A person who doesn't know and pretends to know, is fool, leave him


Bless me in my undertakings Dear God, grant me victory and I shall shout your blessings for all to hear of your power!

Wednesday, January 13, 2010

Hesabu na sayansi katika shule za msingi na sekondari Tanzania

Kumekuwa na changamoto nyingi kuhusiana na namna ambavyo tunaweza kuboresha ufaulu katika masomo ya sayansi na hesabu katika shule za msingi na sekondari. Njia mbalimbali zimetumika pasipo mafanikio. Lakini tafiti nyingi hivi sasa zinaonyesha kwamba tatizo kubwa la kushindwa kwa watoto wetu katika masomo ya hesabu na sayansi yamechangiwa sana na mambo makuu yafuatayo;

  • Hamasa ya masomo ya sayansi na hesabu (motivation). Walio wengi wanaosoma sayansi na pengine wanafaulu vizuri, huishia kuwa na maisha ya shida kuliko wale waliosoma masomo ya sanaa. Kwa kuzingatia hilo wazazi wengi wanawahamasisha watoto wao kuachana na sayansi na kuchagua masomo ambayo yataleta unafuu katika maisha yao. Kazi nyingi zinazohusisha sayansi zinaonekana kutopewa umuhimu mkubwa ama na serikali au jamii inayotuzunguka.
  • Ukosefu mkubwa sana wa walimu. Nataka kukuambia katika zile shule za kata zilizojengwa na hasa zile za mikoani, walimu wa Jiografia ndio wanaofundisha hesabu. Hapo unatarajia mtoto afaulu vipi? Shule zilizobahatika kuwa na walimu basi ni form six leaver ambao hawakubahatika kwenda chuo, wanajitolea kwa kulipwa kiasi kidogo, na utakuta shule yenye mikondo 12 ina mwalimu huyo mmoja tu. Niambie anawezaje kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanajifunza na kuelewa wanachojifunza.
  • Maisha ya walimu ni jambo lingine pia; ualimu umepoteza value katika jamii ya sasa. zamani ilikuwa kuwa mwalimu ni dili na unajivunia kuitwa mwalimu. Lakini hivi leo mwalimu ni kama laana. Kutokana na hali hiyo walimu wengi hawatumii muda wao vizuri kwa ajili ya kazi hiyo ya ualimu, na wanatafuta namna nyingine ya kuyafanya maisha yao kuwa rahisi. wengi hivi sasa wanaamua kujiendeleza kielimu (ni jambo zuri, lakini wanafanya hivyo ili mwisho wa siku wapate kazi nyingine inayolipa zaidi). Matokeo ya hili walimu wengi wamekimbilia kwenye kazi zingine, na hivi sasa mabenki yamejaa walimu, uwanja wa ndege, hali ya hewa na kwingineko kwingi. (wazo lako la kuwaongezea kipato linaweza kuwa zuri lakini, shida inaweza isiwe kipato, bali heshima ya taaluma ya ualimu)
  • Lakini kibaya kuliko yote na mitaala. Kadri tunavyojitahidi kubadili mitaala yetu na kuamini kwamba tunaiboresha, ndivyo tunavyoifanya migumu zaidi na isiyojifunzika. Kuna mapungufu mengi yapo katika suala zima la mitaala; 1. Mitaala yetu mingi inapoandaliwa, haiwashirikishi walimu vya kutosha; kwa kawaida walimu ndo wanaojua matatizo ya wanafunzi na ndo wanaojua ni nini wanahitaji ili wajifunze vema. Lakini walimu wanapewa nafasi ndogo sana katika suala zima la uandaaji wa mitaala. La pili, mitaala haiwapi nafasi walimu kuboresha au kubadilisha jambo lolote katika ufundishaji au content (No teachers creativity and innovations are welcomed). Pengine hili linashawishi decentralized system of education kuliko hii centralized ambayo kuna mtu anaitwa TIE kazi yake kuwaambia wenzake wafanye hiki na kile ambacho yeye mwenyewe hafanyi na wakati mwingine hakijui. 2. Kila mwalimu kazini anafanya kazi yeye kama yeye kuwezesha somo lake lifanikiwe. Hakuna utamaduni wa walimu kushirikiana katika kufundisha. Katika utafiti uliofanyika hivi karibuni Uholanzi, Japan na USA, umeonyesha kwamba walimu wakishirikiana katika kuandaa somo na katika ufundishaji, kunakuwa na ufanisi mkubwa zaidi. 3. Mitaala yetu haiandaliwi kwa kufuata mahitaji yetu ya sayansi kitaifa. Ni kama vile mitaala tunayotumia ni ile tuliyorithi kwa wakoloni. Mtoto wa mkulima, unayemtaka baada ya kumaliza shule yake arudi kuwa mkulima bora, na aweze kuwaelekeza wengine kuhusu kilimo, unamfundisha matrix au integration ili imsaidie nini? Mitaala yetu bado haijatoa kipaumbele cha elimu gani, kwa ajili ya nani na kwanini?
  • Different treatments (nimeshindwa kuipeleka kwenye kiswahili sahihi); Katika post iliyotangulia nimeiita hii "Education of the Rejected in Tanzania". Mtakaopata nafasi mnaweza kutembelea kuona ni nini ninachokiongelea hapa. wanafunzi wanaosoma kigoma, lindi, chunya na kibasila au bunge, na kwingineko nchini wote hufanya mtihani mmoja. Hii haiwatendei haki kabisa watoto wa wakulima kule vijijini ambao wanasoma katika shule zisizo na madawati, maabara, vitabu wala walimu (as the case katika shule zetu za kata). Wengine hawakuwahi hata kumwona huyo mtu anaitwa mwalimu wa hesabu tangu waanze form one hadi form four. Mwisho wa siku wanakaa kufanya mtihani sawasawa na yule ambaye tangu anaanza form one hadi form four ana walimu watano wa hesabu, ana maabara ya sayansi na ana maktaba ya vitabu. Hapa unategemea nini? Ni haki tu kuwa na asilimia 70 ya failures katika hesabu nchini kwakuwa asilimia 80 ya watanzania wanaishi vijijini na huko ndiko kwenye shule mbofumbofu za watanzania waliopuuzwa na kukataliwa nchini kwao. Hapa linaibuka jambo lingine tena ambalo sipendi nilijadili leo, lakini ni vizuri in the future lijadiliwe. kwamba ni nini mstakabali wa watanzania maskini wanaopata elimu duni ya shule za kata ambazo kwazo serikali inajizolea sifa? Maana hawa walioko huko wanapoteza miaka minne bila kugain chochote. Hatma yao ni nini baada ya kumaliza masomo yao huko? Ndo linakuja suala la kwamba sehemu kubwa ya watu walio katika taaluma ya ualimu ni watoto wa wakulima, kwa kuwa hao ndo wanasoma katika mazingira duni na ufaulu wao huwa si wa kuridhisha sana kiasi cha kuwawezesha kujiunga katika fani za waliofaulu sana. Na mbaya zaidi serikali yetu ilishaufanya ualimu kama taaluma ya waliofeli, najua wengi mtanipinga lakini hilo lina ukweli mwingi tu (fanyeni utafiti juu ya hilo.
Lakini la ziada sasa hivi kuna suala la technolojia katika elimu. ICT in Education, ambayo tafiti nyingi zimeonyesha kwamba inaweza kuboresha ufaulu katika sayansi. Lakini kibaya ni kwamba ni asilimia chini ya 20 tu ndo inapata umeme nchini? Zaidi ya asilimia 80 ya watanzania hawana umeme na ndivyo ilivyo kwa shule zao. Je unategemea mwisho wa safari mnaandaa wasomi wa namna gani? Wote hawa watakwenda chuo kikuu mwisho wake; mwingine ana ujuzi wa ICT mwingine hajui. Je kuna haki yoyote wanayotendewa hawo waliokosa nafasi ya kupata elimu kwa njia ya technolojia? Na kama hatuwatendei haki ni watanzania wa aina gani tunaowaandaa?

Bado tuna safari ndefu sana ya kulikomboa taifa letu kielimu. Kuna mawazo mengi mazuri, lakini bado yana mapungufu mengi sana. Wazo la television kwa mfano, bado litawasaidia wachache sana na kuwaacha wengi ambao tayari ni masikini na wanahitaji elimu ili kujikomboa na umaskini wao na wa taifa pia. kuhusu kujenga chuo kikuu cha ualimu wa hesabu wala sioni sababu kwa kuwa vyuo vikuu vilivyopo hivi sasa tu vina nafasi nyingi tu kwa ajili ya walimu wa sayansi lakin havipati applicant wa kutosha or wenye sifa. kwa hiyo kujenga chuo kingine ni wastage of resources. La mishahara nishalijibu, lakin pia la kufundisha hesabu wasio walimu wa hesabu sidhani kama linaweza kuwa na matunda mazuri sana kwa kuwa tayari katika shule nyingi za kata hesabu zinafundishwa na walimu wa jiografia na hata wa kiingereza. You can imagine. Sikubaliani na suala la kuchangia elimu kwa kuwa sina uhakika na matumizi ya bajeti kubwa ambayo wizara ya elimu inatengewa kila mwaka. Sidhani kama inatumika ipasavyo. Kwa hiyo kuchangia kunaweza kuwanufaisha tu watu fulani.

No comments: